UTUMISHI NA UTAWALA
Idara ya Utawala na Utumishi ni nguzo kuu katika kuhakikisha uwajibikaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali ili kufikia dira na malengo ya Halmashauri Ya Wilaya Ya Mvomero. Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali watu wenye weledi, uwezo na mtawanyiko sawia katika maeneo mbalimbali ya kiutawala ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ina idadi ya Tarafa 4 ambazo ni Mgeta, Mlali,Turiani na Mvomero, kata 30 za Bunduki,Langali,Mgeta,Nyandira,Tchenzema,Kikeo Luale,Mlali,Mzumbe,Lubungo,Melelela,Mangae,Msongozi,,Homboza,Doma,Kibati,Pemba,Kweuma,Mhonda,Mtibwa,Kanga,Mziha,Sungaji,Maskati,Kinda,Dakawa,Mvomero,Hembeti,Mkindo na vijiji 130. Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ina jumla ya watumishi 3,226 katika idara 13 za Utawala na Utumishi, Elimu Msingi, Elimu Sekondari, Afya, Mipango Kilimo Umwagiliaji na Ushirika, Mifugo na Nyuki, Maendeleo ya Jamii, Ardhi,Usafi na Mazingira, Fedha, Maji na Ujenzi na vitengo sita (6) ambavyo ni Kitengo cha Manunuzi, Sheria, Ukaguzi wa Ndani, Uchaguzi, Nyuki na Tehama.
Shughuli Zinazofanyika
Shughuli kuu zinazofanyika katika idara ya utawala na utumishi ni pamoja na kuajiri, kupandisha madaraja, kusimamia masuala ya kinidhamu ya watumishi , kuunda bajeti ya utumishi (kusimamia ikama ya watumishi) , usafishaji wa taarifa za kiutumishi, kutatua kero na malalamiko ya watumishi ikiwa ni pamoja na madai yao, kusimamia malipo na makato mbalimbali katika mishahara ya watumishi.
Mafanikio
Mafanikio katika idara ya Utawala na Utumishi ni kama vile kupunguza kero na malalamiko ya watumishi kwa kiasi kikubwa ikiwa ni zao la usimamizi wa misingi ya utawala bora katika Utumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Changamoto
Pamoja na mafanikio vilevile Idara ya Utawala na Utumishi inakabiliana na changamoto zifuatazo ni baadhi ya watumishi kutozingatia sheria, kanuni na taratibu, kasi ya upatikanaji wa watumishi ni ndogo hususani kada ya afya na madai ya watumishi kutolipwa kwa wakati muafaka,Kukosekana kwa ofisi na nyumba za watumishi za kutosha katika vituo vya kazi.
Matarajio
Idara ya Utawala na Utumishi inatarajia kuwekeza katika kujenga mazingira rafiki ya kazi kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati,kuongeza idadi ya ofisi na makazi ya watumishi katika ngazi ya kata na vijiji.Kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa watumishi ili kutoa huduma bora . Vile vile inalenga katika kuhakikisha mtawanyiko sahihi wa watumishi katika maeneo mbalimbali ya kiutawala ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.