Wananchi wanaochukua pikipiki kwa mikataba ya makubaliano na wamiliki wake wameshauriwa kuhakikisha wanashirikisha viongozi wa serikali za vijiji wakiwemo watendaji wa Vijiji ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima pamoja na ukiukwaji wa masharti ya mkataba.
Ushauri huo umetolewa Disemba 08, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto wakati akizungumza na Maafisa Wasaririshaji (Boda boda) wa Kata za Mzumbe na Mlali.
Mhe. Maulid Dotto ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la malalamiko kati ya wamiliki wa pikipiki na waendeshaji wanaochukua vyombo hivyo kwa mkataba bila kuwepo kwa usimamizi wa serikali za vijiji.
Aidha, amesema kuwa ushirikishwaji wa uongozi wa kijiji utasaidia kuweka kumbukumbu sahihi za makubaliano, kuongeza uwajibikaji, na kuhakikisha pande zote mbili zinazingatia taratibu zilizowekwa. Hata hivyo, hatua hiyo itarahisisha utatuzi wa migogoro iwapo kutatokea uvunjifu wa masharti ya mkataba.
Kwa upande wake Askari Kata wa kata ya Mazumbe Afande Selenda amewashauri Maafisa Wasafirishaji hao kutunza kumbukumbu za malipo wanayofanya kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri ili kuepusha migogoro ya inayoweza kutokea.
Nao baadhi ya Maafisa wasafirishaji hao wamesema kuna baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekuwa sio waaminifu na wengine wamekuwa wakiweka masharti magumu, huku akiongeza kuwa wengi wao wanaingia mikataba hiyo kwa sababu wamekosa shughuli nyingine za kufanya ili kujiingizia kipato.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.