Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wameshauriwa kuhakikisha katika vishikwambi vyao ambavyo vimenunuliwa na Halmashauri, wanakuwa na nyenzo nne muhimu zitakazowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi na kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo katika maeneo yao ya uwakilishi.
Ushauri huo umetolewa Disemba 5, 2025 na Katibu Tawala Wilaya ya Mvomero Bw. Said Nguya kwenye hafla ya uzinduzi wa Baraza la kwanza la Madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Katibu Tawala huyo amesema kuwa nyenzo hizo muhimu zitawaongoza waheshimiwa madiwani katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Bw. Nguya ametaja nyenzo hizo ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM 2025 - 2030, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Bunge la 13 na nyenzo ya nne ni ahadi za Mhe. Rais.
Aidha, amewasisitiza kutumia muda wao kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao hii itawasaidia kutambua kero zinazowakabiri wananchi wao, huku akimpongea Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vishikwambi hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Paulo Faty amesema Halmashauri hiyo imejipanga kuishi kidigitali kwa kununua vishikwambi kwani itasaidia kupunguza gharama za kuchapisha vitabu vya taarifa za vikao.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Sarah Msafiri Ally amepongeza hatua hiyo kwani dunia sasa ipo viganjani kutokana na kukua wa sayansi na teknolojia. Pia, amewapongeza waheshimiwa Madiwani kwa kuchaguliwa kuwakilisha wananchi huku akiahidi kutoa ushirikiano ili Halmashauri hiyo isonge mbele.
Nao Waheshimiwa Madiwani akiwemo Mhe. Hamidu Zuberi ambaye ni Diwani wa Kata ya Lubungo ameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuendelea kutekeleza majukumu kwa kipindi ambacho hawakuwepo huku akiahidi kwa niaba ya madiwani kutoa ushirikiano katika kuwahudumia wananchi.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.