Wananchi wa Kitongoji cha Mtakuja, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, wamelipuka kwa furaha na mshangao baada ya kuonekana kwa mnyama adimu aina ya kakakuona, tukio ambalo limezua hamasa kubwa katika jamii na kuchukuliwa kama ishara ya neema katika msimu huu wa mvua.
Kakakuona huyo ameonekana kwa mara ya kwanza usiku wa kuamkia leo katika eneo la Bw. Juma Mwanaguma baada ya kubaini kuwa ni mnyama adimu, alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji na baadaye kwa mamlaka za wilaya kwa mujibu wa taratibu.
Akizungumza leo baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto amewashukuru wananchi kwa kutimiza wajibu wao na kutoa taarifa kwa wakati, akisema kitendo hicho kinaonesha uelewa mzuri wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa mnyama huyo pindi anapoonekana huonyesha ishara mbalimbali kulingana na mila na desturi za jamii, huku akibainisha kuwa Kakakuona huyo ameonesha ishara ya uwepo wa mavuno mengi hususan katika mazao ya mahindi na mpunga baada ya kumuwekea mbegu za mazao hayo, hivyo hakutakuwa na balaa la chakula.
Kwa upande wake Bw. Juma Mwanaguma amesema kuwa mwanzoni alidhani ni mnyama aina ya Nyegere ambaye huwa anavamia maeneo hayo na kuchukua kuku lakini baada ya kugundua kuwa ni Kakakuona ndipo alipoanza kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo hilo, pia ameeleza kuwa ni mara yake ya kwanza kumuona mnyama huyo kwani alikuwa akihadithiwa tu na kuangalia kwenye luninga.
Naye, Mzee Mathei Malunga ameeleza kuwa baada ya kumuona Kakakuona huyo walichukua hatua ya kumuwekea mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo mpunga, mahindi, mtama na kunde ambapo mnyama huyo amechagua mpunga na mahindu huku akisema kuwa inaashiria kuwa kwa msimu ujao wa kilimo unatarajiwa kuwa na mavuno mengi ya mazao hayo.
Afisa Wanyamapori wilaya hiyo Bi. Avelin Maingu amebainisha kuwa katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Kakakuona ameonekana zaidi ya mara tano na kuongeza kuwa hiyo ni ishara ya neema katika Wilaya hiyo.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.