Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amesisitiza kuwa zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 halipaswi kuchukuliwa kwa misingi ya dini wala itikadi za kisiasa.
Mhe. Nguli ameyasema hayo Oktoba 17, 2024 wakati akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la KKKT ushirika wa Dakawa ikiwa ni ziara yake ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la makaazi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema jukumu la kushiriki katika mchakato huo ni la kitaifa na linawahusu wananchi wote bila kujali tofauti zao huku akiongeza kuwa zoezi la kujiandikisha linatoa fursa kwa kila mwananchi kutimiza haki yake ya kidemokrasia na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa taifa.
Hata hivyo alitoa wito kwa viongozi wa dini na wanasiasa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa.
Sambamba na hilo Mhe. Nguli amehimiza wananchi kutumia fursa hii ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi na kufanya maamuzi yanayoathiri mustakabali wa taifa.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi".
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.