Wilaya ya Mvomero imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuinua afya ya jamii na kuongeza nafasi ya wilaya hiyo kufanya vizuri katika tathmini ya kitaifa ya usafi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa Agosti 20, 2025 wakati wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ngazi ya Wilaya kilicholenga kujadili utekelezaji wa kazi mbalimbali za Divisheni ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe mwaka 2022 - 2025, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Akizungumza wakati wa kufunguka kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto amesema kuwa usafi wa mazingira ni ajenda ya kipaumbele, hasa ikizingatiwa kuwa mazingira machafu yanachangia kwa kiasi kikubwa milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo na malaria.
Aidha, Mhe. Maulid Dotto ameongeza kuwa kama Wilaya inatakiwa kuwa na mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa inafanya vizuri kwenye kipengele cha usafi wa mazingira huku akitaja baadhi ya mikakati itakayosaidia kufikia lengo hilo.
"...tuongeze juhudi za kuhakikisha tunashinda katika mashindano tunayoshiriki yanayohusu usafi wa mazingira...lakini pia tuwe na lengo letu kama wilaya na kwa mwaka huu tumekubaliana kwamba tunatoka kwenye namba 83 tushike namba 50..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Baadhi ya mikakati iliyoahinishwa na Mkuu wa Wilaya ni pamoja na kuanzisha siku maalum ya usafi wa mazingira ambayo italenga kuhimiza usafi, kufanya ziara za kushtukiza kwenye maeneo mbalimbali Wilayani humo, Mashindano ya usafi baina ya vijiji, kata, shule na masoko, ambapo washindi watapewa zawadi na kutangazwa hadharani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty amesema kuwa kwa mashindano ya mwaka huu Halmashauri imeweka lengo la kushika nafasi ya 50 akiahidi kuwa lengo hilo litafikiwa.
Naye, Afisa Afya wa Wilaya hiyo Bw. Morgan Towo ameeleza kuwa baadhi ya maeneo bado yana changamoto ya watu kujisaidia porini, ukosefu wa vyoo vya kisasa na uhifadhi hafifu wa taka za majumbani na masokoni, mikakati imewekwa kuhakikisha inabadilika.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.