Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wamefanya ziara ya kimkakati katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kilimo cha kakao na kuongeza tija kwa wakulima wa zao hilo katika wilaya yao. Ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima wa kakao wa Mvomero, kwani imefungua fursa mpya za kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato cha wakulima.
Ziara hiyo iliyoanza Januari 2, 2025 imehusisha kikao cha mafunzo na maonyesho ya teknolojia mpya za kilimo cha kakao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, ambayo inasifika kwa uzalishaji wa kiwango kikubwa na cha ubora wa kakao nchini. Madiwani hao walipata nafasi ya kujifunza kuhusu mbinu za kisasa za upandaji, usimamizi wa mashamba, uchakataji wa mazao, na mbinu za kufikia masoko ya kimataifa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Jailos Msigwa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, amesema kuwa wamejifunza mambo mengi ambayo yatahamasisha mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo cha kakao Mvomero. Ameongeza kuwa mikakati madhubuti itachukuliwa kuhakikisha wakulima wa kakao wanapatiwa mafunzo na vifaa bora vya kilimo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mhe. Ambakisye Njelekela amewashukuru Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kuichagua wilaya yao kama eneo la mafunzo na kubainisha kuwa ushirikiano kati ya wilaya hizo mbili utasaidia kukuza kilimo cha kakao kitaifa.
Naye Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mohammed Longoi amesema Halmashauri hiyo ina kitalu cha zao hilo la Kokoa ambapo msimu wa mwaka 2023/2024 ilizalisha miche 2700 ambayo iligawanywa kwa wakulima lakini mwitikio wake haukuwa mkubwa. Aidha, amebainisha kuwa kwa msimu wa mwaka 2024/2025 wakulima wameonesha kuwa na mwamko mkubwa. Sambamba na hilo amewapongeza Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kujitoa kujifunza kilimo cha zao hilo ili kuhakikisha kuwa maisha ya wakulima yanabadilika.
Akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa zao la kokoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Afisa Kilimo wa Halmashauri Mhandisi Arnold Ngaiza amesema kuwa Kilimo cha kokoa kimekuwa chanzo kikubwa kimojawapo cha kipato cha Halmashauri hiyo akitolea mfano msimu wa mwaka 2023/2024 Halmashauri imekusanya mapato kiasi cha shilingi Bilioni 2.1. Aidha, Mhandisi Arnold amesema Wilaya hiyo inazalisha mazao matatu ya kimkakati yakiwemo mazao ya Kakao, michikichi na mpunga.
Kwa ziara hii, Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wameonesha dhamira ya dhati ya kuinua uchumi wa wakulima na kuboresha hali ya maisha kupitia kilimo cha kakao.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.