Kutokana na malalamiko na vilio vya wakulima wa zao la mpunga Mkoani Morogoro wakilalamikia kutopata faida katika zao hilo, sasa neema imewafikia wakulima hao baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuigiza Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula - NFRA kununua mpunga huo kwa shilingi 900.
Akizungumza na wakulima wa zao hilo wa Kata ya Dakawa Agosti 26, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli wakati akitoa taarifa kwa wakulima juu ya uwepo wa NFRA katika Kata hiyo amewataka kujitokeza ili waweze kuuza mpunga wao.
Mhe. Nguli amesema lengo la Serikali ya Rais Samia ni kuhakikisha kuwa kila mkulima anapata faida na kuinuka kiuchumi kupitia shughuli kilimo anayoifanya ndiyo maana amesikia kilio cha wakulima wa mpunga kutokana na bei isiyo rafiki kwa wakulima badala yake hali zao zimekuwa chini.
"...hawa watajitambulisha muwapokee, mfanye nao biashara.." amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amekea tabia ya baadhi ya Wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi na kwamba kodi hizo ndiyo zinazo saidia Halmashauri kuboresha huduma za jamii kama shule, maji na huduma za afya.
Naye Msimamizi wa Maghala kutoka NFRA Bw. Paul amesema wanatekeleza agizo la Rais Samia la kununua mpunga kwa shillingi 900 kwa kilo huku akiwaomba wakulima hao kutoa ushirikiano. Pia amesema mkulima atakatwa kodi ya asilimia 2 kwa ajili ya TRA na asilimia 3 itakakwa NFRA kwa ajili ya mapato ya Halmashauri.
Kwa upande wao wakulima akiwemo Bw. Nasibu Katoto ameishukuru NFRA kwa kuja kununua mpunga huo huku akiomba elimu zaidi itolewe hususan kwenye tozo ya asilimia 2 ambayo mkulima anatakiwa kulipa. Aidha amesema kwa bei hiyo ya shilingi 900 kwa kilo ni bei nzuri na kwamba inambeba mkulima ukilinganisha na bei za wanunuzi wengine.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.