Zaidi ya shilingi milioni 679 zimetolewa kwa vikundi 79 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu wilayani Mvomero, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuwezesha wananchi kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji mikopo hiyo Wilayani Mvomero iliyofanyika leo Januari 10, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Judith Nguli amemuagiza Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kuhakikisha kuwa hadi kufikia siku ya jumatano ya Wiki ijayo vikundi hivyo vinapata fedha hizo ili viendelee na shughuli za uzalishaji.
“...kuhakiki tu unaweza kutumia jumamosi, jumapili, jumatatu...ikifika jumatano sisi tunacheka...” amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Nguli amewaagiza Maafisa ugani wa Kata, Maafisa biashara, maafisa maendeleo ya jamii pamoja na watendaji wa Vijiji na Kata kuhakikisha kuwa wanavisimamia vikundi hivyo pamoja na kuwapatia elimu juu ya miradi wanayobuni ili fedha zilizotolewa zilete tija.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya wanufaika dhidi ya matumizi mabaya ya mikopo hiyo, akiwahimiza wawekeze katika miradi yenye tija kama kilimo, ufugaji, na biashara ndogo ndogo ili kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya wilaya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Halmashauri zote hapa nchini kutoa mikopo hiyo. Aidha, Mbunge ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kutenga fedha za asilimia 10 kutoka kwenye Makusanyo yake kwa ajili ya kuwainua wananachi kiuchumi.
Awali akitoa taarifa ya tathmini ya vikundi vilivyoomba mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mashaka Malole amesema jumla ya vikundi vya wanawake 57 vinatarajia kupata kiasi cha shilingi milioni 428.4, vikundi vya vijana 17 watapata shilingi milioni 218.5 na vikundi vya wenye ulemavu ni vinne ambavyo vitapata shilingi milioni 24.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo akiwemo Bi. Jackline Mwaisiga mkazi wa Kata ya Mzumbe akiwakilisha kundi la watu wenye ulemavu amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulikumbuka kundi hilo la wenye ulemavu, akisema kuwa kupitia mikopo hiyo itawawezesha kujiinua kiuchumi na kushiriki katika fursa ambazo awali walikuwa hawashiriki.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.