Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeielekeza Wizara ya Kilimo kuvunja mkataba wa ukarabati wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgongola iliyopo katika Kata ya Mkindo kutokana na kutoridhishwa na utekelezaji wake.
Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kufanya ukaguzi Februari 16, 2025 kwenye mradi huo na kubaini dosari mbalimbali, zikiwemo mkandarasi kushindwa kutimiza masharti ya mkataba ikiwemo kukamilisha mradi kwa wakati.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Mariamu Ditopile Mzuzuri amesema kuwa licha ya serikali kutenga fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya kuimarisha skimu hiyo, utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
"...huu mkataba kwanza umeshaisha kwahiyo kwa mujibu wa sheria uende ukavunjwe na kama kuna hasara yoyote imeenda aidha kwa Serikali ama kwa wananchi iende ikalipwe ipasavyo na huyu mkandarasi..." amesema Mhe. Mzuzuri.
Aidha, Kamati hiyo imemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji kufika mara moja katika mradi huo ili kuangalia mradi pamoja na kufanya maboresho katika mkataba mpya kama utasainiwa kuhakikisha kuwa eneo la uzalishaji linaongezeka kufikia hekta 1500 pamoja na marekebisho ya chanzo cha maji ili kuongeza uwezo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema lengo la Mkoa ni kuifanya skimu hiyo kuwa ya mfano wa kilimo cha mpunga nchini kwa kufanya maboresho ya chanzo ili kuongeza eneo la uzalishaji wa kilimo shadidi kutoka hekta 620 hadi hekta 1500 na kukaribisha wawekezaji kwenye hekta 1500 zilizobaki kuendelea kuongeza uzalishaji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya skimu hiyo.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Morogoro kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Juma Mattanga amebainisha kuwa mkandarasi alianza kazi tarehe 7 Septemba, 2022 na muda wa kukamilisha mradi ilipaswa kuwa tarehe 6 Septemba, 2023 lakini mkandarasi aliongezewa siku 120 hivyo ulitakiwa kukamilika tarehe 6 Januari, 2024 hadi sasa mradi huo upo asilimia 44 ya utekelezaji na kazi imesimama.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.