Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto ametoa siku saba kwa Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji vyote vya Kata ya Dakawa kwa kushirikiana na Viongozi wa chama cha wafugaji na viongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji kuhakikisha kuwa wanaondoa na kuzuia mifugo yote inayoingia katika skimu umwagiliaji ya Ushirika wa Wakulima Wadogo wadogo wa mpunga Dakawa (UWAWAKUDA) kuanzia Disemba 17 hadi 24, 2025.
Mhe. Dotto ametoa agizo hilo Disemba 17 wakati wa kikao cha wadau wa UWAWAKUDA ambacho kimefanyika katika Ofisi za ushirika huo, kabla ya kikao hicho Mkuu huyo wa Wilaya ametembelea na kukagua eneo la shamba hilo na kujionea uharibifu wa miundombinu uliyofanywa na mifugo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu huyo wa Wilaya amesema uvamizi wa wafugaji umesababisha uharibifu wa miundombinu, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na kupunguza tija ya uzalishaji wa mazao.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Skimu hiyo Bw. Nasibu Katoto amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa agizo hilo huku akisisitiza kuwa kila mtendaji kwa nafasi yake asimamie sheria na kutekeleza wajibu wake ipasavvyo.
Kwa upande wake, Meneja wa UWAWAKUDA Bi. Irene Calist ameeleza kuwa uwepo wa mifugo katika eneo hilo umekuwa ukisababisha uharibifu wa mifereji ya maji, mashamba ya wakulima na kusababishia harasa kwani hutumia zaidi ya milioni 300 kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 24 kwa ajili wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo uzalishaji uliongezeka kutoka gunia 10 hadi gunia 40 kwa hekta.
Diwani wa Kata ya Dakawa Mhe. Joshwa Makukula ameushauri uongozi wa skimu hiyo kushirikisha viongozi wa Vijiji katika kamati zao za ulinzi na usalama ili kuongeza nguvu katika ulinzi wa shamba hilo, pia amewataka kuona namna ya kukusanya masalia ya majani na kuyahifadhi na kuyauza kwa wafugaji husasan kipindi cha kiangazi na kwamba itasaidia kuondoa adha hiyo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.