Machi 09, 2024 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imepokea ugeni kutoka Baraza la Wawakilishi likiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Machano Othman Said pamoja na Kamati ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika ziara ya ukaguzi wa mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mfumo wa Ikolojia Vijijini (EBBAR) uliopo katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Waziri Harusi amekagua mradi wa lambo kwa ajili ya kuvunia maji lenye thamani ya Sh. 293,654,565.32 ambalo linatumika kumwagilia ekati 4 za zao la nyanya kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji wa matone, pia bwawa hilo linanufaisha wananchi kwa uwepo wa samaki aina ya sato ambao wamepandikizwa katika bwawa hilo.
Pia amekagua ujenzi wa kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi wenye thamani ya Sh. 108,010,000.00 ambao utanufaisha vijana kwa kujiajiri na mradi wa shamba la uzalishaji uyoga wenye thamani ya Sh. 5,500,000 katika Kijiji cha Melela kata ya Melela.
Waziri huyo na Kamati ya Wajumbe wa Baraza pia walitembelea katika Kijiji cha Mingo kilihopo Kata ya Lubungo na kukagua mradi wa kisima kirefu cha umwagiliaji wa mazao ya mbogamboga kwa kutumia umeme wa nguvu za jua (Solar) wenye thamani ya Sh. Milioni 22.
Waziri amesema “...mradi huo umewapatia wananchi wa Wilaya ya Mvomero manufaa makubwa kwa kuweza kupata ajira ambayo inawasaidia katika kuendesha maisha yao ya kila siku”.
Aidha amewataka wasimamizi wa mradi huo kuendelea kuutunza na kuudumisha ili uendelee kuleta manufaa zaidi kwa wananchi na kuwarahisishia kupata huduma za kijamii zikiwemo maji yanayowasaidia katika shughuli za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ofisi ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Mhe. Machano Othmani Said amesema mradi huo utawasaidia wananchi kujikwamua na umaskini na kuwarahisishia kupata huduma za kijamii kwa urahisi, hivyo amewataka wananchi kuitunza miradi hiyo ili iweze kudumu na kuwasaidia kujipatia kipato na huduma za jamii hususan maji kutokana na uwepo wa visima na malambo yaliyopo katika maeneo hayo.
Mhe. Machano amewataka wananchi waendelee kuthamini mchango wa Serikali zote mbili (Muungano) katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Wilaya ya Mvomero ni moja kati ya Wilaya zinazotekeleza mradi wa Kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBBAR), mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF). Wilaya nyingine zinazotekeleza mradi huu Tanzania Bara ni Mpwapwa (Dodoma), Simanjiro (Manyara) na Kishapu (Shinyanga) kwa upande wa Zanzibar ni Matemwe (Unguja).
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.