Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB) amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli upatikanaji wa mbegu bora za malisho kwa ajili ya mashamba 1,200 ya Wafugaji ambao wamekubali kujiunga kwenye Kampeni ya Tutunzane Mvomero.
Mhe. Kijaji ameyasema hayo Januari 4, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Mvomero pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kwa ajili ya ziara ya kikazi Wilayani humo.
Waziri huyo amesema changamoto inayowakabili wafugaji wengi ni suala la malisho ya uhakika na maji hususan wakati wa kiangazi, hivyo amesema Wizara itahakikisha mbegu hizo zinapatikana ili mashamba hayo 1200 ya wafugaji yapandwe na kwamba yatasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.
“...narejea Naibu Katibu hili la mbegu tulale, tuamke lazima mbegu zipatikane za malisho...sisi sasa ndio muda wetu wa kutokulala na kutokuota mpaka tutakapo hakikisha wafugaji wote, mashamba yote 1200 yamepata mbegu..." amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji amesema zoezi hilo la ugawaji wa mbegu ni kuungamkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliizindua kampeni hiyo Agosti 3, 2024 hivyo watahakikisha hawamuangushi.
Sambamba na hilo amewataka wafugaji kufuga kisasa ili mifugo yao iwe na viwango vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa huku akibainisha kuwa Mkoa wa Morogoro utakuwa kanda maalum ya mifugo na kwamba mapinduzi ya Sekta hiyo yataanzia Mkoani Morogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amebainisha mipango ya Mkoa huo kwenye sekta ya mifugo ikiwemo kuufanya mnada wa Mkongeni kuwa Soko la kimataifa la mifugo huku akisema kuwa ili kufikia huko wafugaji wanatakiwa kuwa na mifugo yenye viwango.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amesema upatikanaji wa mbegu za malisho pamoja na gharama za uchimbaji wa visima ni changamoto mojawapo katika utekelezaji wa kampeni hiyo. Aidha, amesema wakati kampeni hiyo inaanza kulikuwa na mashamba 379 ambayo yalipatiwa hati lakini kutokana na kukosekana kwa mbegu yalipandwa mashamba 42 pekee, hadi sasa wafugaji 1202 wamehamasika kuandaa mashamba.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.