Watumishi mbalimbali wa Wilaya ya Mvomero wakiongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ndg. Frazier Mangula wamejumuika kwa pamoja kufanya usafi wa mazingira katika eneo linalozunguka Hospitali Kuu ya Wilaya hiyo eneo la Makao Makuu ya Wilaya.
Shughuli hiyo ni utekelezaji wa moja ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika Disemba 9 mwaka huu.
Watumishi hao wakiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Phillipina Phillipo, walishiriki kwa pamoja kufyeka vichaka na nyasi, kung’oa visiki, pamoja na kuondoa taka nyingine ngumu katika eneo linalozunguka hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala amewaasa watumishi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika usafi wa mazingira kwa kuhakikisha wanafuata maelekezo ya Serikali inapotoa maagizo mbalimbali huku akisisitiza kwamba tarehe 9 Disemba ambayo ni kilele cha Maadhimisho wa Siku ya Uhuru wa Tanzania bara kwa pamoja watumishi na wanachi watashiriki kupanda miti katika maeneo mbalimbali ambayo yatachaguliwa.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kiasi cha Shilingi Milioni 960 ambazo zilipangwa kutumika katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Uhuru katika ujenzi wa mabweni 8 katika shule za Msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hii inaonesha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa rais kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.