Watumishi wa Divisheni ya Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa haki.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Paulo Faty wakati wa kikao kazi kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na uboreshaji wa utoaji huduma katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa vitendo vya rushwa vinadhoofisha jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya na vinaathiri moja kwa moja ustawi wa wananchi, hususan wale wa kipato cha chini.
“...lakini nisisitize kwenye tabia binafsi kataeni rushwa...kuikataa rushwani pande mbili kuitamani na pale inapotolewa kupokea...usitamani rushwa, usipokee rushwa..." amesema Ndg. Paulo Faty.
Aidha, amewapongeza watumishi hao kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi wa Wilaya hiyo licha ya uchache wa watumishi uliopo huku akiongeza kuwa ataendelea kuiomba Serikali kuongeza watumishi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Chuma Novacatus, amesema kuwa Hospitali hiyo ilianza kujengwa mwaka 2015 kwa fedha kutoka Seikali kuu ambapo hadi sasa ina majengo 14 kati ya majengo 28. Aidha, amesema kuwa Hospitali hiyo inatoa huduma mbalimbali za kibingwa ikiwemo huduma za uzazi na watoto, huduma za magonjwa ya macho na miwani, huduma za kinywa na meno, huduma za maabara, huduma za dharula, huduma za mionzi, kifua kikuu na ukoma, huduma za magonjwa ya kinamama na upasuaji na huduma za ustawi wa jamii.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.