Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwajibikaji, na uadilifu ili kumsaidia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa Februari 20, 2025 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuph Makunja wakati akifungua mkutano wa kawaida wa baraza la Madiwani lililolenga kujadili taarifa za Robo ya Pili kwa kipindi cha Oktoba - Desemba 2024, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Makunja amesisitiza umuhimu wa kila mtumishi kujituma na kufanya kazi kwa bidii katika idara yake ili kuhakikisha maendeleo ya Wilaya na ya wananchi yanapiga hatua.
"...naomba ndugu zangu wataalam na watendaji wa Halmashauri fanyeni kazi ile ambayo inayotakiwa katika shughuli zetu za kawaida na maelekezo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania..." amesisitiza Mhe. Makunja.
Aidha, amewataka Watumishi wa Halmashauri hiyo kutoa ushirikiano kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Loema Peter ambaye ameaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwatumikia wananchi wa Mvomero.
Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo wa Halmashauri amempongeza Mkurugenzi kwa maono mazuri ambayo anaamini yataivusha Halmashauri hiyo kwenda kwenye hatua nyingine ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewaomba Waheshimiwa Madiwani kumpokea Mkurugenzi huyo mpya na kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa malengo ya Halmashauri yanatimia.
Mhe. Nguli amewasisitiza Watumishi na watendaji kumsaidia na kupokea mabadiliko, mipango na mikakati ya kuitoa Halmashauri hiyo mahali ilipo sasa na kuipeleka kwenye Mvomero ya mafanikio.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.