Watendaji wa kata na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, wameagizwa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.
Agizo hilo limetolewa leo Februari 14, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Loema Peter wakati wa kikao kazi cha Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na Mapitio ya mfumo wa Mapato (FFARS) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Bi. Loema amesema kuwa serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ujenzi wa shule, zahanati, barabara, na miradi ya maji, hivyo ni jukumu la watendaji wa ngazi za chini kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo.
“...mradi wowote uliopo kwenye kipande chako hicho ulichopewa kama ni kijiji, kama ni Kata ule mradi unakuhusu...unakaaje pembeni wakati upo nyumbani kwako...” amesisitiza Mkurugenzi.
Aidha, amewataka watendaji hao kufuatilia miradi yote na kutambua kama miradi hiyo ni ya Serikali au ya watu binafsi na wananchi wa eneo hilo wananufaikaje na hiyo miradi.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa pamoja na majukumu mengine watendaji wanajukumu la kulinda Amani na utulivu katika maeneo yao.
Katika Hatua nyingine, Bi. Loema amewata watendaji wa kata na Vijiji kusimamia mapato na matumizi katika maeneo yao huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa sheria watendaji wanatakiwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi kila baada ya miezi mitatu.
Kwa upande wao, baadhi ya watendaji wa kata na vijiji waliohudhuria kikao hicho wameahidi kutekeleza maelekezo hayo kwa bidii na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa Mvomero inaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.