Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Marry Kayowa kwa niaba ya Msimamizi w Uchaguzi wa Halmashauri hiyo amewataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kuwa waadilifu, makini, na kufuata sheria, kanuni, na taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na haki.
Bi. Marry Kayowa ameyasema hayo Novemba 22, 2024 wakati akifungua kikao cha mafunzo kwa Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura kwa Tarafa ya Turiani na Mvomero yaliyofanyika katika ukumbi wa Community Centre uliopo katika Kata ya Mtibwa.
Msimamizi huyo Msaidizi wa Uchaguzi amesisitiza kuwa jukumu la usimamizi wa uchaguzi ni la kipekee na linahitaji uwajibikaji wa hali ya juu ili kudumisha imani ya wananchi kwa mchakato mzima wa uchaguzi.
"...msingi wa kwanza ni uadilifu lakini uaminifu lakini kuna uwajibikaji...kwahiyo hatutatarajia na hatufikirii kwamba miongoni mwetu au baadhi wakaenda kinyume na yale tunayoelekezwa..." amesema Bi. Marry Kayowa.
Aidha, amewakumbusha wasimamizi hao kuwa jukumu lao linaambatana na dhamana kubwa, na yeyote atakayekiuka maadili na taratibu atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja wasimamizi wa vituo kutoka Tarafa ya Turiani na Mvomero huku lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.