Wasimamizi Wakuu na Wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wa Serikali za Mitaa 2024 wametakiwa kutanguliza uzalendo na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wa uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano Novemba 27, 2024.
Wito huo umetolewa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya Bi. Mary Kayowa wakati akifungua Semina ya siku moja kwa Wasimamizi Wakuu na Wasimamizi wasaidizi wa Vituo vya kupigia kura kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza na wasimamizi hao, Msimamizi huyo amesema kuwa jukumu walilopewa ni nyeti na linahitaji uadilifu wa hali ya juu ili kulinda haki za wapiga kura na kuimarisha demokrasia katika taifa.
"...lakini tunapaswa kufahamu kuwa jambo hili ni nyeti na maslahi yake hayafanani na jambo ambalo tunaenda kulifanya, ni jambo linaloonesha uzalendo wetu sisi..." amesema Mary Kayowa.
Aidha, Bi. Mary ameonya dhidi ya matumizi ya lugha zisizofaa kwa wananchi ambao watajitokeza kupiga kura na kwamba hatarajii kuona wasimamizi hao wanakiuka sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji, hasa katika masuala ya utaratibu wa kupiga kura, kuhesabu kura, na kutangaza matokeo kwa uwazi.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.