Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wananchi wametakiwa kuendelea kudumisha amani na utulivu pamoja na kuwapuuza watu wanaochochea uvunjifu wa amani iliyopo.
Wito huo umetolewa leo Aprili 26, 2025 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero Ndg. Said Nguya wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano ambapo kiwilaya maadhimisho hayo yamefanyika katika shule ya Sekondari Sokoine Memorial.
"...tuwapuuze wale ambao wanaleta chokochoko kwa maslahi yao binafsi, nchi yetu imeendelea kuwa kisiwa cha amani tangu enzi za Waasisi wetu Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume, tuitunze tunu hiyo..." amesema Ndg. Nguya.
Aidha, amewataka vijana kuwa makini na watu ambao wamekuwa wakiwashawishi vijana kufanya vulugu kwa maslahi yao ya kisiasa huku akiwataka kuripoti taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mohamed Longoi akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amewashukuru Viongozi, Watumishi, Wanafunzi pamoja na wananchi waliojitokeza kuadhimisha sherehe za Muungano kwa kushiriki kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo usafi na upandaji miti.
Sambamba na hilo, amewahimiza wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu 2025.
Naye Kaimu Afisa elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Shangweli ameushukuru uongozi wa Wilaya na Halmashauri kwa kuchagua shule ya Sekondari ya Sokoine Memorial kuadhimisha sherehe za Muungano ngazi ya Wilaya. Aidha, amewataka walimu na wanafunzi kutunza miti ambayo imepandwa shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mwaka huu 2025 zimepambwa na kaulimbiu isemayo "Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano: Muungano wetu ni dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025..."
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.