Wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana wadau ili kuleta matokeo chanya kwa kuongeza uzalishaji, ubora na usindikaji wa mazao ya mifugo, kilimo na uvuvi.
Wito huo umetolewa Agosti 2, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki 2024 uliofanyika katika viwanja vya maonesho vya Mwl. J. K. Nyerere vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema wananchi wakiongeza uzalishaji itasaidia nchi kuendelea kuwa na usalama wa chakula na lishe bora, kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwandani, kuongeza mazao nje ya nchi, kuongeza ajira kwa wananchi pamoja na kuchochea mchango wa Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwenye pato la Taifa.
"...wito wangu kwenu ni tuendelee kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau ili kuleta matokeo chanya..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, amebainisha kuwa Sekta hizo zina mchango katika upatikanaji wa ajira kwa wananchi ambapo zaidi ya asilimia 65 ya watanzania wanajishughulisha na sekta hizo, vile vile zinachangia asilimia 28 ya pato la Taifa pia zinachangia asilimia 24 ya mauzo ya bidhaa zinazotokana na mazao ya sekta hizo nje ya nchi. Lakini pia zina imarisha usalama wa chakula na lishe bora.
Sambamba na hilo, Dkt. Buriani ameeleza mikakati ya Seikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto zilizopo kwenye Sekta hizo ikiwemo uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Rufiji Meja Edward Kiwele akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amesema maonesho ya Nane nane kanda ya mashariki 2024 lengo lake ni kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza mbinu mbalimbali za teknolojia mpya zinazoongeza tija na kuleta mabadiliko chanya katika sekta hizo muhimu kwa usalama wa chakula na uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa hadi kufikia Julai 30, 2024 zaidi ya washiriki 596 wamethibisha kushiriki katika maonesho hayo kwa mwaka huu ikilinganishwa na washiriki 589 mwaka 2024 huku akisema kuwa watu zaidi ya 80000 wanatarajiwa kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Maonesho ya Nane nane 2024 kitaifa yanafanyika Mkoani Dodoma huku yakiwa na kaulimbiu isemayo "Chagua Viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.