Wananchi wa Wilaya ya Mvomero wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu ya kibingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya hiyo, huduma hizo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuboresha afya za wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila mtu.
Wito huo umetolea mapema hii leo Oktoba 16, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli wakati wa uzinduzi wa Kambi Maalum ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia awamu ya pili inayoendelea katika Hospitali ya Wilaya pamoja na kukabidhi gari kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za afya.
Mhe. Nguli amesema kuwa matibabu hayo yatahusisha wataalamu bingwa kutoka sekta mbalimbali za afya, wakiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, upasuaji, magonjwa ya Wanawake na uzazi, usingizi na magonjwa ya watoto pamoja na magonjwa ya kinywa na meno huku akisisitiza kuwa huduma hizo zitakuwa za gharama nafuu na zingine zitatolewa bure ili kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya matibabu.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kutumia nafasi hii muhimu kujitokeza kwa wingi na kuhamasishana kwani Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imewasogezea huduma karibu na kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu na gharama kubwa kufuata huduma za kibingwa katika hospitali kubwa.
Sambamba na hayo, Mhe. Nguli amewataka wajumbe wa timu ya usimamizi wa huduma za Afya katika hospitali hiyo (CHMT) kutumia gari walilokabidhiwa kama ilivyokusudiwa na hatimaye kuleta matokeo chanya katika huduma hizo za Afya.
Awali wakati akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni amesema uwepo wa Madaktari Bingwa wa Mama Samia imekuwa ni faraja kwa wananchi wa Wilaya hiyo kwani imerahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa karibu na wananchi hao.
Aidha, Mwl. Linno amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya katika Wilaya hiyo hususan katika hospitali ya Wilaya na kwamba Halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Wilaya hiyo.
Naye, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Alex Mzava amesema wamepokea Madaktari Bingwa saba huku akibainisha kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa kwani tangu kuanza kwa kambi hiyo wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi.
Kwa upande wake Dkt. Beatus ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya kinywa na meno, kwa niaba ya Madaktari hao amesema lengo la uwepo wao ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi wa Wilaya ya Mvomero pamoja na kuwajengea uwezo Madaktari waliyopo katika hospitali hiyo ili kuendeleza huduma hizo pindi wao watakapo ondoka.
Madaktari Bingwa wa Mama Samia wameanza kutoa matibabu ya kibingwa katika hospitali ya Wilaya kuanzia Oktoba 14 na wataendelea hadi Oktoba 20, 2024.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.