Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameendelea kuwahimiza wananchi Wilayani Mvomero kuchangamkia kilimo cha mazao ya viungo kwa kuwa yanafaida katika kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Dkt. Mussa ametoa wito huo Mei 9, 2024 wakati wa zoezi la ugawaji wa miche 500 ya Karafuu kwa wananchi wa Vijiji vya Mnyanza na Tangeni vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kuhamasisha wananchi Mkoani Morogoro kulima mazao ya viungo kama vile Karafuu, Vanila, kokoa, Iriki na Mdalasini.
Katibu Tawala huyo amesema lengo la Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi – CCM ni kuboresha maisha ya watanzania kupitia nyanja mbalimbali kama vile kilimo, hivyo amewataka wananchi wa Vijiji vya Tangeni, Mnyanza na maeneo mengine kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ambazo zinalenga kuboresha maisha yao.
“...maneno yetu yachukueni na ninyi fanyeni kwa sababu tunachokifanya ni kuwaachia rasilimali ambayo itawasaidia ninyi wenyewe na vizazi vyenu...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amebainisha uwepo wa masoko ya uhakika wa mazao hayo ya viungo.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo ameendelea kuwasisitiza wakulima kuwakwepa madalali ambao wamekuwa mwiba kwa wakulima kushindwa kufikia malengo ya kukuza uchumi.
Naye Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya Mvomero Bi. Consolata Tarimo amesema Wilaya ya Mvomero ni miongoni mwa Wilaya zinazolima zao la Karafuu ambapo hadi sasa Wilaya imepokea miche 1000 ya zao hilo ambayo imegawanywa katika vijiji vya Mnyanza, Tangeni na vijiji vingine vinavyozalisha karafuu.
Ameongeza kuwa Halmashauri imeanzisha kitalu cha miche ya karafuu 12000 katika Kata ya Mhonda huku akibainisha kuwa wananchi wamelipokea kwa mikono miwili zao hilo la Kimkakati.
Kwa upande wao wananchi waliopokea miche hiyo akiwemo Bw. Mustafa Salum ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo ambayo itainua uchumi wao. Pamoja na kuipongeza Serikali Bw. Mustafa amemshukuru Katibu Tawala huyo kwa kuhakikisha kuwa wananchi Mkoani Morogoro wananufaika na kilimo cha mazao ya viungo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.