Wananchi wametakiwa kuepuka tabia ya kugomea au kupinga utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwao na taifa kwa ujumla, bali washirikiane kikamilifu na Serikali pamoja na wadau ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa na kuleta matokeo chanya katika ustawi wa uchumi wa jamii.
Wito huo umetolewa Julai 16, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Me. Maulid Dotto wakati akizungumza na Viongozi pamoja na wananchi wa kijiji cha Gonja.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa miradi ya uwekezaji ikiwemo mradi wa uboreshaji wa msitu wa Kijiji cha Gonja unaotekelezwa na Shirika la PAMS Foundation unalenga kutoa fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi hivyo ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa kijiji hicho kuacha tabia ya kuzuia miradi kama hiyo ambayo itawanufaisha wananchi wengi.
"...mradi huu wa PAMS Foundation unafursa nyingi za kiuchumi na kijamii tuache kuzuia zuia vitu ambavyo vinakwenda kusaidia watu..." amesema Mhe. Maulid Dotto.
Aidha, ameongeza kuwa zipo sheria mbalimbali za utunzaji wa mazingira, ardhi na misitu ambapo kila kiongozi, mwananchi anawajibu wa kuzifuata na kuzitekeleza.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Viongozi wa Serikali ya kijiji cha Gonja na wananchi wa kijiji hicho kuupokea kwa mikono miwili mradi wa uboreshaji wa msitu wa Kijiji hicho ili waweze kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty amesema kuwa wananchi ndiyo wenye maamuzi katika matumizi ya rasilimali za vijiji kupitia mkutano Mkuu wa Kijiji huku akibainisha kuwa Serikali ya kijiji haina mamlaka ya kufanya maamuzi bila mkutano mkuu wa wananchi.
Naye Afisa Misitu kutoka Halmashauri hiyo amesema kuwa Mkuu wa Wilaya aliunda timu ya kupitia upya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji hicho na kutoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo uwekaji wa alama za kudumu katika mipaka ya msitu huo ili kuzuia uvamizi unaofanywa na wananchi.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.