Wananchi Wilayani Mvomero wameaswa kuchangia huduma ya maji inayopatikana katika maeneo yao na kwamba fedha hizo wanazochangia zinasaidia katika kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwenye maeneo husika.
Wito huo umetolewa Mei 20, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuph Makunja wakati akifungua Warsha ya mradi wa kuboresha huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Makunja amesema kuwa Serikali imetumia gharama katika kuwapelekea wananchi wake huduma ya maji safi na salama hapa nchini ili waondokane na matumizi ya maji yasiyo salama kwa afya zao lakini baadhi ya wananchi wanaharibu miundombinu hiyo na kugoma kulipia huduma hiyo muhimu huku akisema kuwa kitendo hicho ni kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Aidha, Mweyekiti huyo amewataka wananchi kuipa kipaumbele huduma ya maji kutokana na umuhimu wake katika maisha ya mwanadamu.
“...tusimame kama viongozi wa Serikali tuwape mafunzo wananchi wetu, tuwape maelekezo ikiwezekana tuweze kulipia maji kabla ya matumizi ili tuondokane na changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo yetu...” amesema Mhe. Makunja.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Sekta binafsi katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na kuanzisha mradi wa kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira Wilayani humo.
Naye, Mratibu wa zoezi la ushirikishwaji jamii katika mpango wa Serikali wa ushirikishaji Sekta binafsi katika miradi ya maji Vijijini Bw. Emmanuel Burton amesema zoezi hilo la usshirikishwaji jamii linafanyika katika mikoa mitano ya Kagera, Morogoro, Lindi, Dodoma na Manyara ambapo Wilay 15 zimechaguliwa kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo.
Aidha, Bw. Burton amebainisha changamoto ambazo zimepelekea kushindwa kufikia lengo la asilimia 85 katika upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ambapo kwa sasa wamefikia asilimia 77, changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa rasilimali fedha, upungufu wa rasilimali watu. Pamoja na hayo amesema wananchi kushindwa kuchangia huduma ya maji kunapelekea ugumu katika uboreshaji wa miundombinu ikiwemo mabomba na vichotea maji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya watumia maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Ezdonia Batholomeo amewashukuru wawezeshaji wa warsha hiyo ambapo amesema itasaidia kuboresha vyombo vya watumia maji vilivyopo Wilayani humo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.