Wananchi wa vijiji vya Lubungo na Mingo ambavyo vipo Kata ya Lubungo Tarafa ya Mlali Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro vyenye jumla ya wananchi wapatao 2016 wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mradi wa maji na hivyo kuondokana na adha ya maji.
Kabla ya mradi huo walilazimika kutembea kilomita zaidi ya 10 kufuata maji kwenye mito na mabwawa huku wakihatarisha maisha yao kwani eneo hilo linapakana na Mbuga ya Mikumi eneo ambalo lina wingi wa tembo.
Hayo yameelezwa na Diwani wa Kata ya Lubungo Hamidu Zuberi kwenye ufunguzi wa Mradi wa maji wa Lubungo ulioghalimu zaidi milioni 400 fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maji (NWF) na kutekelezwa na RUWASA.
Alisema utekelezwaji wa Mradi huo umeenda kumshusha Mama ndoo kichwani kwa sasa wananchi hawachangii tena maji na Tembo kama hapo awali na kwamba wameshapoteza wapendwa wao 4 na wengine kupata ulemavu wakati wakienda kwenye mito na mabwawa.
“Nimshukuru sana Mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha hizi za mradi wa maji kata ya Lubungo kiukweli Mama ametuheshimisha mimi pamoja na Mbunge wangu Mhe. Zeeland sasa tunapita kifua mbele.” alisema Mheshimiwa Diwani.
Akizungumza kwenye mkutano wa adhara na wananchi wa Kata ya Lubungo Waziri wa Maji Jumaa Aweso aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla kuwa Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya maji itahakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama.
Aidha aliwataka wananchi walio karibu na mradi wa maji kuulinda na kuutunza ili waendelee kupata huduma ya maji safi na salama kila wakati kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo ili wananchi waweze kupata maji.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilayani Mvomero, Mhandisi Sospeter Lutonja akitoa taarifa juu ya mradi huo alisema kuwa mradi huo umetekelezwa na Kampuni ya CHAKWELE CO. LTD ulianza 04.10.2018 na kukamilika rasmi 22.11.2021 unahudumia wananchi zaidi ya 2000. Mradi huo umegahrimu kiasi cha shilingi za Kitanzania 417,078,804.52 ambapo mkandarasi tayari ameshalipwa kiasi cha shilingi 406,460,795.18.
Utekelezaji wa mradi huo ulijumuisha ujenzi wa tanki la maji ujazo wa 90,000, mnara wa mita 6, ununuzi na ulazaji wa mabomba umbali wa mita 4020, ujenzi wa vituo 16 vya kuchotea maji pamoja na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya nishati ya jua 9KW.
Hisani : RUWASA Tanzania / Farida Mangube
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.