Wananchi wa Kitongoji cha Majichumvi wametoa shukrani zao kwa Shirika la Rotary kwa msaada mkubwa wa kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama katika kitongoji hicho ambapo shirika hilo limechimba kisima ambacho kinatoa lita 20000 kwa masaa mawili mradi ambao umegharimu dola za Marekani 5200.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo wa maji leo Septemba 27, 2024 katika Shule ya Msingi Majichumvi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Dakawa Mhe. Yusuf Makunja amesema mradi huo umeleta faraja kubwa kwa wakazi wa kitongoji hicho ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.
Aidha, Mhe. Makunja amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo huku akiliomba kuendelea kutoa msaada katika maeneo mengine yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
"...kwa hesabu za haraka haraka haya maji yamepatikana kwa milioni 13 na pointi za kitanzania, ela si ndogo sisi tunawashukuru sana..." amesema Mhe. Makunja.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makunja akiwa kama Diwani wa Kata ya Dakawa ameahidi kuchangia umaliziaji na ukarabati wa ofisi ya walimu katika shule ya Msingi Majichumvi.
Naye, Mwakilishi wa shirika la Rotary amesema Rotary ni shirika la Kijamii linajihusisha na kusaidia maendeleo ya jamii pia kila mtu ana nafasi ya kujiunga ikiwa tu analengo la kuisaidia jamii kimaendeleo, shirika hilo linajumuisha watu wa kada mbalimbali ambapo huchangishana fedha ambazo zinapelekwa kwenye jamii yenye uhitaji.
Ameongeza kuwa mradi wa kisima katika kitongoji cha Majichumvi umegharimu kiasi cha dola 5200 za Marekani ambazo ni sawa shilingi milioni 13 za kitanzania. Hata hivyo, ameahidi kuwa Rotary itaendelea kutoa ushirikiano ili kuleta maendeleo katika jamii.
Miongoni mwa wananchi waliotoa shukrani zao kwa shirika hilo ni pamoja na Bi. Immaculata Charles mkazi wa Kitongoji cha Majichumvi amesema changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ilipelekea wao kutumia maji ya miferejini ambayo sio salama kwa afya zao.
Nao wanafunzi wa Shule ya Msingi Majichumvi akiwemo Subira Rafael ameshukuru kupata huduma hiyo ya maji ambayo itawasaidia kutumia muda mwingi kusoma.
Katika hafla hiyo ya kukabidhi mradi wa maji kwa wananchi Mhe. Diwani pia alikabidhi jezi seti moja pamoja na mpira mmoja kwa timu ya vijana ya kitongoji hicho.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.