Ni muda mfupi tangu kuanzishwa kwa kampeni ya Tutunzane Mvomero ambapo hadi sasa zaidi ya wafugaji 702 wamehamasika kujiunga na kampeni hiyo ambayo imelenga kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na utunzaji wa mazingira.
Hayo yamebainishwa Agosti 1, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli wakati wa kikao cha wadau wa Sekta za mifugo na kilimo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Nguli amesema tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo imewezesha wafugaji hao 702 kupimiwa ardhi na kupata hati zao, aidha, ameongeza kuwa kuna mashamba 42 ambayo yamepandwa malisho huku akibainisha kuwa changamoto iliyopo ni upatikanaji wa mbegu kwa ajili ya wafugaji wengine wenye mashamba kupanda malisho yao.
Pia amesema ujio wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unatarajiwa kuwa suluhu ya changamoto hiyo ya mbegu.
“...zaidi ya wafugaji 702 wamo kwenye kampeni ya tutunzane, sasa tuna idadi kubwa ya watu waliohamasika kwa muda mfupi...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hilo, Mhe. Judith Nguli amebainisha kuwa Kampeni hiyo sasa itakuwa endelevu kwani umeandaliwa mpango wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka huu 2024 hadi 2028 lengo ni kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inawafikia wafugaji wengi ili kumaliza kabisa migogoro katika Wilaya hiyo. Pia ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano mzuri tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi ameipongeza Wilaya ya Mvomero kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kupambana na migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutumia mbinu za kisayansi. Aidha, ameeleza mikakati ya Serikali katika kukabiliana na wingi wa mifugo hapa nchini ikiwemo kuhimiza wafugaji kuvuna mifugo yao ili waweze kuihudumia kwa urahisi.
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Shekhe Twaha Kilango amempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo kwa ushirikiano anao utoa kwa viongozi wa dini pamoja na kamati za Maridhiano katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji huku akisema kuwa Amani na utulivu uliopo Mvomero kwa sasa ni matokeo ya ushirikiano uliopo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.