Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewataka wadau wa maendeleo Wilayani humo kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam wa ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kufanikisha mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi ardhi ambao unatarajia kufanyika Wilayani humo.
Mhe. Nguli ameyasema hayo Aprili 22, 2024 wakati akifungua Mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi Wilayani Mvomero uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa wadau hao wanaifahamu vizuri Wilaya hiyo kuliko wataalam wa wizara hivyo amewataka kutoa maoni, ushauri na mapendekezo chanya ambayo yatasaidia kupunguza au kuondoa kabisa migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo.
“...naomba mtumie nafasi hii kutoa maoni, mapendekezo na mambo muhimu yanayohitajika katika mahitaji yetu halisi kwenye maeneo yetu…” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Judith Nguli ametumia mkutano huo kuipongeza na kuishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuanzisha mradi huo ambao ni tiba ya migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiipa sifa mbaya Wilaya hiyo. Ameongeza kuwa Vijiji 40 Wilayani humo vimeingizwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Naye, Afisa Mipango miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Paul Kitosi Amesema mradi huo umebuniwa na Serikali ya Awamu ya sita ukiwa na lengo la kusimamia milki za ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini huku akibainisha kuwa mradi huo unafadhiliwa na mkopo kutoka Benki ya dunia ambapo zaidi ya shilingi bilioni 346 zimekopwa kutekeleza mradi huo. Ameongeza kuwa mradi huo ni wa miaka mitano na ulianza mwaka 2022 na utakamilika 2027.
Aidha, amesema mradi huo umezingatia usawa wa kijinsia huku akisema kuwa mradi huo lengo lake kuu ni kupanga, kupima na kumilikisha viwanja milioni mbili mijini na vijijini hapa nchini.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bunduki Mhe. Prosper Mkunule ameishukuru Serikali ya awamu ya sita pamoja na Mkuu wa Wilaya kwa kuwa msikivu kwa wananchi wa Wilaya hiyo, aidha amesema mradi huo ni muhimu katika Wilaya hiyo kwani utaupa heshima Wilaya kwa kuwa migogoro ya ardhi itapungua au kuisha kabisa.
Mkutano huo wa wadau wa ardhi unaenda sambamba na kauli mbiu isemayo “usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi kwa ustawi wa jamii”.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.