WAANDIKISHAJI WASAIDIZI NA WAENDESHA VIFAA VYA BAYOMETRIKI WASISITIZWA KUWA MAKINI KATIKA UANDIKISHAJI WA MAJINA YA WAPIGA KURA
Posted on: February 27th, 2025
Waandikishaji wasaidizi na waendeshaji wa vifaa vya bayometriki katika ngazi ya kituo wamesisitizwa kuwa makini katika uandishi wa majina ya wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kuepuka makosa yanayoweza kuathiri haki ya raia kushiriki katika uchaguzi.
Msisitizo huo umetolewa leo Februari 27, 2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omar Ramadhani Mapuri wakati wa mafunzo ya waandikishaji hao, yaliyofanyika katika ukumbi wa Prof. Kuzilwa uliopo Kata ya Mzumbe.
Mhe. Balozi Mapuri ameeleza kuwa usahihi wa majina ni muhimu katika kuhakikisha kuwa kila mpiga kura anaweza kutumia haki yake ya kikatiba bila vikwazo.
"...muhakikishe kwamba majina mnayaandika kwa usahihi na hilo ni muhimu sana sana..." amesisitiza Mhe. Balozi Omar Ramadhani Mapuri.
Sambamba na hilo, Mjumbe huyo amewakumbusha waandikishaji hao kuwa na ushirikiano na mawakala wa vyama vya siasa akibainisha kuwa mawakala hao watasaidia kutambua wakazi halisi wa maeneo yao.
Naye, Afisa Muandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura Jimbo la Mvomero Bi. Mary Kayowa amesema kuwa Jimbo hilo linajumla ya vituo 348 huku akibainisha kuwa washiriki waliopatiwa mafunzo hayo kwa ni 816, ambapo washiriki 408 ni waendesha vifaa vya Bayometriki na 408 ni waandishi.
Ameongeza kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamefundishwa mada mbalimbali ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu wapiga kura ambalo linataanza rasmi kuanzia tarehe 1 Machi hadi Machi 7 2025.
Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha kuwa mchakato wa uandikishaji wa wapiga kura unafanyika kwa uwazi, usahihi na kwa kuzingatia taratibu zote za uchaguzi.
Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linaambatana na kaulimbiu isemayo "Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora"