Katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na maonesho ya Nane Nane hata baada ya kufungwa rasmi, viwanja vya Nane Nane vilivyopo Katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, vinatarajiwa kuwa soko la kudumu la bidhaa mbalimbali zikiwemo mboga mboga, nyama choma pamoja na matunda pia ni eneo la kutoa shamba darasa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Hayo yamebainishwa Agosti 8, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian wakati akizungumza na Viongozi pamoja na wananchi kwenye kilele cha Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. J. K Nyerere vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa mpango huo unatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuwainua wakulima wadogo na wajasiriamali kwa kuwawezesha kuuza bidhaa zao moja kwa moja kwa walaji huku akiwataka wananchi kuendelea kutembelea viwanja hivyo ili waendelee kujifunza.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki 2025 amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza tija na matumizi endelevu ya eneo hilo hususan baada ya Maonesho hayo kuhitimishwa rasmi. Pia, amesema kila siku ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zitakuwa siku mabazo wakulima watauza bidhaa zao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amesema pamoja na uuzaji wa mboga mboga kutakuwa na uwepo wa nyama choma pamoja na maonesho ya wanyama na michezo mingine ya kuvutia.
Naye, Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari amebainisha kuwa Kanda ya Mashariki inachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa Sukari hapa nchini huku akieleza matarajio ya bodi ni kuzalisha tani 756000 za sukari ili nchi iweze kujitosheleza kwa sukari
Maonesho ya Nane nane kanda ya Mashariki 2025 yataendelea hadi Agosti 9, 2025 huku yakiwa na kaulimbiu isemayo "Chagua Viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025"
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.