Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amevitaka vikundi mbalimbali vya Vijana, akina mama na makundi maalum kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kupitia Halmashauri hapa nchini kwa lengo la kukuza mitaji yao pamoja na kuongeza uzalishaji wenye tija.
Mhe. Pinda amesema hayo Agosti 8, mwaka huu kwenye kilele cha Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki 2024 yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu amebainisha wakati akitembelea mabanda amekuta vikundi vingi vinajihusisha na kilimo, ufugaji na uvuvi hivyo, amezitaka Halmashauri kuviwezesha vikundi hivyo kupata mikopo hiyo ili kuongeza mitaji yao.
"... tumevikuta vikundi viko hali ya juu kiuchumi lakini vimetokana na mfuko wa 10% na vingine vinapaswa kuchukua kutekeleza majukumu yao, Wakurugenzi wa Halmashauri waliangalie hilo..." amesema Mhe. Mizengo Pinda.
Aidha, Mhe. Pinda amesema Wakurugenzi wa Halmashauri wanatakiwa kuibua vikundi vitakavyonufaika kutokana na mikopo hiyo na ambavyo vitakuwa rahisi kuvifuatilia ili kuendana na kasi ya kukua kwa teknolojia katika uzalishaji wa mazao ya Kilimo, mifugo na uvuvi.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu huyo Mstaafu amesema sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi zimesaidia kupunguza tatizo la ajira kwa Vijana hapa nchini kwani wamekuwa wakifanya shughuli hizo kama vyanzo vya kujipatia kipato.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mizengo Pinda amesisitiza wananchi kutilia mkazo suala la lishe bora ambapo amewataka kula mlo kamili ikiwemo vyakula vya mboga mboga kuepuka matatizo ya kiafya ikiwemo utapiamlo ambao bado ni changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika ushiriki wa maonesho hayo ya Nane Nane kanda ya mashariki kwa mwaka huu kutokana na kuwepo kwa ubunifu wa teknolojia katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, ambapo yamefanya maonesho hayo kuvutia zaidi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafugaji na wakulima kuwa wa mfano hapa nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa, pamoja na kuishi kwa amani na kuheshimiana huku akiwataka wafugaji kuwa na maeneo yao ya kulishia mifugo ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Maonesho ya nanenane hufanyika kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 8 ambapo mwaka huu yamekuwa na kaulimbiu inayosema " Chagua viongozi bora wa Serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi".
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.