Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Februari 25, 2025 imeendesha mafunzo maalum kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani. Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea ujuzi wa usimamizi wa miradi ili kuongeza ufanisi, tija na urejeshaji wa mikopo kwa wakati.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi. Sia Ngao amesema kuwa serikali inatilia mkazo utoaji wa mafunzo haya ili kuhakikisha mikopo inayotolewa inaleta maendeleo kwa wanufaika na jamii kwa ujumla.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii amewasisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha wanaongeza kipato na kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine wapate fursa hiyo.
Mafunzo hayo yamejumuisha mada mbalimbali kama Kilimo bora na Ufugaji wa Kuku na Nguruwe, ufugaji wa samaki, mbinu bora za ujasiriamali, usimamizi wa fedha, upatikanaji wa masoko, na namna ya kurejesha mikopo kwa wakati.
Nao baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo akiwemo Bw. Mido Rashidi mwanakikundi cha Family Group kutoka kata ya Mlali ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga zaidi kuhusu kilimo bora chenye tija ambacho kitawawezesha kurejesha mkopo waliochukua.
Kwa upande wake Bi. Farida Emily kutoka kikundi cha Kihanu kilichopo Turiani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa hiyo ya mikopo. Pia, ameishukuru Halmashauri kwa mafunzo hayo ambayo yatawaongezea ujuzi katika ufugaji wa kuku wa nyama.
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imesisitiza kuwa itaendelea kutoa mafunzo kama haya kwa wanufaika wa mikopo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika ipasavyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.