Vijiji 5 Wilayani Mvomero vinatarajia kunufaika na mradi wa kupunguza uzalishaji wa Hewa Ukaa (Kaboni) unaotokana na uharibifu wa misitu ikiwemo ukataji na uchomaji wa misitu hovyo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa Aprili 30, 2024 na Meneja wa Uendeshaji kutoka Kampuni ya Village Climate Solution Limited Bw. Aklei Albert wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kilicholenga kuwasilisha mapendekezo ya kuidhinisha rasimu ya makubaliano ya kuanzisha, kutekeleza na kugawana gharama na faida ya mradi wa kaboni kati ya Vijiji vya mradi, Halmashauri na Kampuni ya Village Climate Solutions kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Bw. Albert amesema Mvomero ni miongoni mwa Wilaya zinazotekeleza mradi wa hewa ya ukaa Mkoani Morogoro ambapo mradi huo unatekelezwa katika hifadhi za misitu ya Vijiji 5 vya Maharaka, Kihondo, Misengele, Sewekipera na Msongozi.
Aidha, ameongeza kuwa lengo la mradi huu ni kuwezesha vijiji vinavyomiliki misitu ya asili kunufaika na misitu yao kupitia biashara ya kuuza hewa ya ukaa yaani kaboni.
Naye, Mwanasheria wa Halmashauri hiyo Bi. Cotrida Komba amesema vijiji vya mradi vinatarajia kupata zaidi ya asilimia 60 kupitia biashara ya hewa ya ukaa. Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa taratibu za biashara ya kaboni hapa nchini mikataba ya biashara hiyo inachukua miaka 30 hadi 40 hivyo, Halmashauri hiyo imependekeza iwe kwa kipindi cha miaka 40.
Kwa upande wake Mhe. Christopher Maarifa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amelishukuru shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kupitia Kampuni ya Village Climate Solution Limited (VCSL) kwa kuleta mradi huo katika Wilaya ya Mvomero na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufanikisha mradi huo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.