Katika juhudi za kuinua uchumi wa vijana nchini, Serikali imewataka vijana kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili kuweza kujikwamua kiuchumi. Mikopo hii inalenga kuwawezesha vijana kuibua miradi yenye tija, kuanzisha biashara, na kuongeza fursa za ajira.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Studio ya Muziki katika Kata ya Dakawa Wilayani Mvomero, Katibu Tawala na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo na Sanaa la Wilaya hiyo Bw. @saidnguya amewataka Vijana kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hii ya mikopo ambayo ni moja ya juhudi za serikali kuunga mkono mipango ya maendeleo ya vijana na kuinua hali za kiuchumi za jamii kwa ujumla huku akibainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imetenga zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na wenye ulemavu.
Katibu Tawala huyo amesisitiza kuwa mikopo hii hutolewa kwa masharti nafuu bila riba wala dhama na inalenga kusaidia vijana kutekeleza miradi mbalimbali kama vile kilimo, biashara, ufugaji, na ujasiriamali mdogo.
Katika hatua nyingine, Bw. Nguya amewapongeza Vijana hao kuwa na wazo la kubuni Studio hiyo ambayo ni ya kwanza katika Wilaya hiyo huku akisema kuwa sanaa ni kazi kama kazi nyingine ambazo zinawasaidia watu kujiingizia vipato.
Pamoja na hayo ametoa ahadi ya kulipia gharama za kurekodi muziki kwa wasanii wanne ambao watahitaji kurekodi nyimbo angalau moja lengo ni kuhakikisha kuwa wasanii wa Wilaya hiyo wanafanikiwa katika shughuli zao za sanaa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.