Vijana zaidi ya 200 Wilayani Mvomero wanatarajia kunufaika na mradi wa Kilimo Tija unaolenga kutoa elimu ya kilimo kwa vitendo pamoja na kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo na ardhi kwa ajili ya kulima ili kuwainua kiuchumi.
Hayo yamebainishwa Aprili 24, 2024 na Mkuu wa Wilaya Mvomero Mhe. Judith Nguli wakati akizindua rasmi mradi wa Kilimo Tija Wilayani humo, zoezi hilo la uzinduzi umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
Mhe. Nguli ameeleza kuwa Mradi huo utawanufaisha vijana 200 kutoka Kata ya Lubungo na maeneo mengine ya Wilaya hiyo ambapo watapatiwa Ardhi, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mikopo ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwa mazao ya matango, matikiti maji na mbogamboga.
“...vijana 200 watapata fursa ya kupata uwezeshwaji katika mradi huu kwa maana watapewa ardhi kama ilivyoorodheshwa hapo lakini pia watalima mazao yaliyotajwa kutoka kwenye ekari 100 za SUGECO...” amsema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza SUGECO (Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwainua vijana kwa kuanzisha mradi huo Wilayani humo na kuwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo muhimu kwani itanua uchumi wa vijana wa Wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa pamoja na mradi kuwanufaisha vijana 200 lakini pia utazalisha ajira 1410 kwa vijana huku akibainisha kuwa jambo hilo linaunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha ajira milioni nane hadi kufikia mwaka 2025.
Naye Mkurugenzi wa SUGECO Bw. Revocatus Kimario ameeleza kuwa mradi huo utatekelezwa katika Kijiji cha Lubungo na utakuwa wa miaka mitatu hadi 2027, walengwa ni vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 35. Ameongeza kuwa vijana hao watapatiwa ardhi kuanzia nusu ekari hadi ekari tatu, kupatiwa pembejeo za kilimo, mikopo kutoka taasisi za kifedha, kutafutiwa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi pamoja na kutafutiwa ajira.
Nao wanufaika wa mradi huo akiwemo Bw. John Ruanda ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuweka mazingira mazuri kwa wadau wa maendeleo ambapo imesaidia kupatikana fursa kama zinazotolewa na SUGECO, pia amewataka Vijana kuipokea fursa hiyo kwa mikono miwili ili waweze kujikwamua kiuchumi.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.