Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tawi la chuo kikuu Mzumbe umefanya dua na maombi maalum ya kuliombea Taifa pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi wakiombewa afya njema, hekima na uongozi wenye mafanikio kwa ajili ya maendeleo ya taifa kuelekea uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Dua hiyo imefanyika Februari Mosi, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sekondari Mzumbe, hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Chama, Serikali, wanachama wa CCM, wanachuo na Wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo amewataka vijana kuwa makini na kupinga upotoshaji unaoenezwa na watu wenye nia ovu dhidi ya maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kushiriki katika ujenzi wa nchi kwa kushikamana na kuunga mkono juhudi za serikali.
"...sasa kuna watu wanapotosha hapa anaingia kwenye kundi la vijana hili ndo analijaza sumu badala ya kumuonesha njia..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za msingi ikiwemo za Afya, Elimu, Maji na umeme pamoja na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavuta wawekezaji walete fursa za ajira kwa vijana.
Aidha, amewashukuru Viongozi wa dini Wilayani humo kwa kazi kubwa ya kuliombea taifa pamoja na viongozi wengine usiku na mchana ili amani na utulivu viendelee kudumishwa huku akibainisha kuwa sala na dua ni muhimu katika kuliongoza taifa.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Seneti Mkoa wa Morogoro ndg. Powell Maruma amesema dua hiyo ni ishara ya mshikamano wao na serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa amani na utulivu. Aidha, amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, kushiriki shughuli za maendeleo na kuhamasisha uzalendo.
Kwa upande wake Shekhe wa Kata ya Mzumbe Shekhe Suleiman Mzee amesema ili Taifa liwe salama ni lazima wananchi pia wawe salama kwa kuyaacha matendo yote ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza na kuyatenda yale ambayo yanatakiwa kufanywa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.