Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imepanga kurejesha hadhi ya Mkoa wa Morogoro kuwa wa Viwanda kama ilivyokuwa awali ambapo Mkoa huo ulikuwa na Viwanda vingi.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Agosti 06, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa huo kwenye mkutano wa hadhara akihitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
Rais Samia amesema lengo la kurejesha Viwanda hivyo ni kukuza uchumi wa Mkoa pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
"...Tunataka kurudisha hadhi ya Morogoro ya Viwanda..." amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Dkt. Samia amesema ameshatoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuhakikisha kuwa viwanda vilivyopo havifi na vile vilivyokufa vinafufuliwa ili vianze kuzalisha akitolea mfano Kiwanda cha Vipuri cha Mang'ula na Kiwanda cha mafuta ya kupikia.
Sambamba na hilo, amesema uwepo wa Reli ya SGR na umeme wa uhakika unafanya Mkoa huo kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji huku akiwataka viongozi na wananchi kuacha mivutano badala yake watenge maeneo ya uwekezaji ili kupata wawekezaji wengi.
Naye, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amebainisha kuwa kuwa Mkoa wa Morogoro hususan Manispaa ya Morogoro ni kitovu cha viwanda vingi vinavyochakata bidhaa za kilimo. Waziri Bashe ameongeza kuwa kupitia kiwanda cha Tumbaku na Sigara watu 12000 wataajiliwa hadi kufikia Juni 2025.Waziri huyo wa Kilimo ameeleza kuwa Serikali inatarajia kufufua kiwanda cha Morogoro Farmers ambacho kitazalisha nyuzi za kufungia tumbaku ambazo Serikali huziagiza kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa hivyo hadi kufikia Disemba 2025 kiwanda hicho kitakuwa kimefufuliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo ni Mkoa wa Kilimo huku akibainisha kuwa hata viwanda vilivyopo vinachakata bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo. Aidha, ameongeza kuwa upatikanaji wa umeme umerahisisha uzalishaji katika viwanda vya Mkoa huo.
Rais Samia anatarajia kuhitimisha ziara yake Mkoani Morogoro kwa kuzindua Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.