Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Halmashauri ya Mvomero imepongezwa kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira Wilayani humo kwa kuanzisha vitalu vya miti ili kurudisha uoto wa asili kama ilivyokuwa awali.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 20, mwaka huu na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Ndg. Godfrey Eliakimu Mzava wakati akizindua mradi wa vitalu vya miti katika Shamba la Miti Mtibwa lililopo katika kijiji cha Lusanga Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
Ndg. Godfrey Mzava amebainisha kuwa uharibifu wa mazingira hususani uoto wa asili umepelekea mabadiliko ya tabia ya nchi ambao umechangia ongezeko la joto, mafuriko na majanga mengine, hivyo ameipongeza TFS kwa kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kuwapatia miti na kuipanda katika maeneo yao.
"...wenzetu wa TFS wameanzisha vitalu vya miti pia wanawapatia wananchi ili kurudisha uoto wa asili, Mwenge wa Uhuru umeridhishwa kuona kazi hii inafanyika..." amesema Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Aidha, Kiongozi huyo amewasisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti pamoja na kuhakikisha kuwa shughuli zinazofanyika kama vile za viwandani, kilimo, uvuvi na ufugaji zinaelekezwa katika utunzaji wa mazingira na kwamba wananchi waache tabia ya kukata miti ili kuondokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mwenge huo wa uhuru utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Gairo kesho Aprili 21, 2024.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.