Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS Wilayani humo kwa kuunga mkono Serikali kwa kuboresha huduma za jamii zikiwemo elimu, Afya, maji na huduma zingine muhimu kwani kwa kufanya hivyo kunasaidia jamii kutatua ama kumaliza kabisa changamoto zake.
Mhe. Nguli ametoa pongezi hizo Julai Mosi, 2024 wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya umaliziaji wa Ofisi ya Serikali ya Kijiji Cha Wami Sokoine na ukarabati wa shule iliyofanyika katika Shule ya Msingi Sokoine.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa madarasa na madawati kwa sababu ya ongezeko kubwa la watoto katika shule mbalimbali kutokana na Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo, hivyo amipongeza TFS kwa kujitoa kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na huduma nyingine katika Wilaya hiyo.
*"...mimi niwapongeze sana TFS mmekuwa mfano mzuri kwa sababu kila mwaka mnafanya haya..."* amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, amesema kuwa Taasisi zinazojitoa kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii zinajenga mahusiano mazuri na jamii husika hivyo kurahisisha baadhi ya shughuli za taasisi hizo.
Sambamba na hilo Mhe. Nguli ametoa rai kwa taasisi nyingine kushiriki katika zoezi la kuboresha huduma za jamii kwani sheria na miongozo ya nchi zinahimiza taasisi kuhakikisha kuwa zinarudisha huduma kwa jamii.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa tishio kwa usalama wa watoto.
Naye, Afisa Muhifadhi wa Shamba la Miti Morogoro Bw. Mohammed Kiyangi amesema TFS kupitia Ofisi ya hifadhi ya shamba la miti Morogoro imekuwa na utaratibu wa kuchangia shughuli za maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Ameongeza kuwa hifadhi ilipokea barua kutoka Serikali ya Kijiji cha Wami Sokoine iliyobainisha mahitaji muhimu ya vifaa vya ujenzi kwa ajili ya shule pamoja na umaliziaji wa ofisi ya Serikali ya Kijiji. Hata hivyo, Afisa Muhifadhi huyo amebainisha changamoto zinazoikabili hifadhi ya shamba la miti Morogoro ikiwa ni pamoja na ongezeko la mifugo katika hifadhi ambayo imekuwa ikikwamisha na kurudisha nyuma juhudi za uhifadhi wa msitu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sokoine Mwl. Tambwe Mavumila amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na upungufu na uchakavu wa vyumba vya madarasa ambapo kwa sasa shule hiyo ina madarasa 11 kati ya 33 yanayohitajika huku ikiwa na wanafunzi 1446. Aidha, ameshukuru kwa vifaa hivyo ambapo anaamini itapunguza changamoto ya madarasa huku akibainisha kuwa wanafunzi ni wengi wanakaa chini kutokana na uchache wa madarasa na madawati.
Katika hafla hiyo vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mbao 90 saruji mifuko 88, gypsum bodi vipande 25 na gypsum powder mifuko mitatu vifaa vyote vinathamani ya shilingi 3,002,000.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.