Katika juhudi za kupunguza athari za wanyama waharibifu hususan tembo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Doma kuhusu namna ya kujikinga na madhara ya tembo katika maeneo yao.
Elimu hiyo imetolewa Novemba 09, 2024 na Maafisa wa TAWA na TANAPA katika Ofisi za Kijiji cha Maharaka ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima alilolitoa Oktoba 27, 2024 kwenye ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum) Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika.
Akielekeza baadhi ya mbinu hizo Afisa Mhifadhi Wanyamapori TAWA Bw. Gilbert Magafu amebainisha mbinu mbalimbali zikiwemo za kitamaduni na kisayansi zinazoweza kutumiwa kuzuia tembo kuingia kwenye mashamba na makazi ya watu kama vile matumizi ya pilipili kama njia ya kuwafukuza, matumizi ya mifereji maalum na mabomu baridi.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu David Kadomo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi amesema elimu hiyo inamanufaa kwa wananchi ilikuhakikisha kuwa hawapati madhara yoyote. Ameongeza kuwa kuna Vijiji vinne ambavyo vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kati ya hivyo Vijiji Vitatu Vinachangamoto kubwa ya tembo ambavyo ni Maharaka, Doma na Kijiji cha Mkata hata hivyo Serikali ilipeleka Vijana 10 kwa kila Kijiji kwenye mafunzo ya kufukuza tembo pamoja na kuwafundisha wananchi mbinu za kujilinda na tembo
Elimu hii pia inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kutunza wanyamapori ili kuendeleza utalii wa ndani na kuchangia katika uchumi wa taifa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.