Wananchi wametakiwa kufichua Taasisi zinazotoa huduma za kifedha hususan zinazokiuka misingi ya Leseni katika utoaji wa mikopo kandamizi (mikopo kausha damu) kwa wateja wake pamoja na kuwafanyia vitendo vya uzalilishaji ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.
Wito huo umetolewa Agosti 22, 2024 na Afisa Msimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Jackson Mushumba wakati wa Mafunzo ya usimamizi wa fedha yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Community Centre uliopo Kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.
Bw. Jackson amesema kuwa Taasisi zote zitakazo bainika kukiuka misingi ya utoaji mikopo kama ilivyoelekezwa na Benki Kuu ya Tanzania chini ya Wizara ya Fedha zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa leseni huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Wilaya pindi wanaposhuhudia ukiukwaji wa misingi ya leseni.
“...sheria ipo wazi ni adhabu gani kwa hawa watoa huduma wanaokiuka taratibu, adhabu moja wapo ni pamoja na kufutiwa leseni zao...” amesema Bw. Jackson.
Aidha, amesema Wizara imeboresha mfumo wa kufichua taasisi zinazotoa huduma ndogo za kifedha hususan zinazotoa mikopo kausha damu ambapo taarifa za mwananchi atakayebainisha taasisi hizo zitalindwa.
Katika hatua nyingine, Afisa huyo amewataka wananchi kusajili vikundi vyao ili kuwa na usalama wa fedha zao katika vikundi hivyo.
Naye Bi. Grace Samwel ambaye ni Afisa Usimamizi wa Fedha (Wizara ya Fedha) amewataka wananchi kuyaelewa masharti ya mikopo kabla ya kuchukua mikopo hiyo. Pia, amezitaka taasisi zinazotoa huduma za kifedha kuainisha na kuweka wazi masharti na taratibu za kupata mikopo katika taasisi zao.
Kwa upande wao wananchi akiwemo Bi. Latifa Japhari wakati akichangia mada zilizowasilishwa na maafisa hao, amewashauri wananchi wengine kuwa na tabia ya udadisi ili kubaini kama wanatendewa haki pindi wanapoenda kuchukua mikopo kwenye taasisi zinazotoa huduma za kifedha.
Ikumbukwe kuwa sharia ya mikopo kwa taasisi ndogo zinazotoa huduma za kifedha imeelekeza taasisi hizo kutoza riba isiyozidi asilimia 3.5 katika mikopo inayotoa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.