Skauti Wilayani Mvomero wameadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa Harakati za Skauti Duniani, Sir Robert Stephenson Smyth Baden Powell, kwa kufanya shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali ya jamii.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Februari 22, 2025 katika mazingira ya mshikamano na huduma kwa jamii, ambapo skauti wameshiriki kusafisha Soko la Dakawa, Kituo cha Afya Dakawa, Kituo cha Polisi Wilaya ya Mvomero na kwenye mifereji ya barabara, lengo ni kuonesha dhamira yao ya utunzaji wa mazingira kwa vitendo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kamishna wa Skauti Wilaya ya Mvomero, Mwl. Charles Kajiru amesema kuwa lengo la shughuli hiyo ni kuendeleza maadili ya skauti ya kuwajibika kwa jamii na kutunza mazingira.
Aidha, ameongeza kuwa madhumuni makubwa ni kuhakikisha kuwa vijana wa skauti wanakuwa wasafi kwenye maeneo yao ya nyumbani pamoja na kuifundisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza mazingira. Pia, ametoa wito kwa wananchi Wilayani humo kuwa na tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao.
Sambamba na hilo, Kamishna huyo wa Skauti amewataka vijana kufikisha ujumbe kwa wazazi wao ili waweze kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambapo kwa Wilaya ya Mvomero zoezi hilo linatarajiwa kuanza tarehe 01-07 Machi, 2025.
Nao baadhi ya Vijana wa Skauti walioshiriki zoezi hilo akiwemo Elias kutokea kata ya Dakawa amesema zoezi hilo ni sehemu ya kuenzi maneno ya Mwanzilishi wa Skauti duniani ambapo alisema "acha dunia yangu ikiwa safi na bora".
Maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Sir Robert Stephenson Smyth Baden Powell huadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Februari na skauti kote duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake katika kuanzisha na kuendeleza harakati za skauti duniani.
Kaulimbiu ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mwanzilishi huyo wa Skauti duniani inasema "Skauti toa maoni ya Dira ya Taifa 2050, Shiriki uchaguzi Mkuu 2025"
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.