Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ameongoza mamia ya viongozi wa Serikali pamoja na wananchi katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Tanzania yaliyofanyika katika Kijiji cha Mvomero, Kata ya Mvomero tarehe 24.07.2023.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya aliwakumbusha wananchi umuhimu wa wao kujitoa kwa ajili ya taifa lao na kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuiga mfano wa mashujaa waliolipigania taifa mfano akiwa Koplo Fokas Emmanuel kutoka Wilaya ya Mvomero.
“Leo tunaadhimisha siku hii Kiwilaya. Naomba tuwaunge mkono mashujaa wetu. Kwa sisi sasa hivi, tulipiganie taifa kwa matendo. Tunahitaji wazalendo kwenye Wilaya yetu kama Koplo Fokas Emmanuel. Tuwaepuke walio na nia mbaya na Wilaya yetu.”aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande mwingine, mmoja wa askari aliyepigana vita ambaye pia ni mwananchi wa Wilaya ya Mvomero Kapteni Mstaafu Kiloko mwenye umri wa miaka 77 amewaasa vijana kuwa na umoja na kutoogopa kujiunga na jeshi kwani si gumu kama wanavyohadithiwa.
“Wakati wa Vita ya Kagera, Watanzania wote walishiriki kumuondoa Nduli Amin Dada kwa namna yao. Kila mmoja alichangia alichonacho. Wengine kuku, mchele yote katika uzalendo wa nchi yao” aliongeza Kapteni Mstaafu Kiloko.
Akitoa salamu kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Yusuph Makunja aliwataka wananchi kuwa na imani na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani kupitia yeye ameendelea kuwaletea Wana-Mvomero viongozi bora na wachapakazi mfano akiwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Judith Nguli.
Katika Maadhimisho hayo, viongozi Serikali, dini na wanajeshi wastaafu waliweka zana mbalimbali za jadi kwenye mnara wa Kumbukumbu wa mmoja wa mashujaa Koplo Fokas Emmanuel ikiwa ni kuthamini jitihada na mchango wa askari waliopambana kwenye vita ya ukombozi wa taifa. Zana zilizosimikwa ni pamoja na mkuki, ngao,mshale, shoka na mashada ya maua kama ishara ya kuwaenzi mashujaa wa Tanzania.
Maadhimisho hayo pia yaliendana na kufanya usafi katika kituo cha Afya Mvomero ambapo viongozi, watumishi wa kituo hiko pamoja na wananchi walijumuika pamoja kufanya usafi eneo linalozunguka kituo hiko.
Eneo la Mvomero kuna mnara wa mmoja wa askari mashujaa aliyeshiriki kwenye vita ya ukombozi wa nchi Koplo Fokas Emmanuel aliyefariki dunia wakati akilipigania taifa vitani tarehe 10.4.1979.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.