Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imepongeza juhudi za Shirika la SAWA WANAWAKE TANZANIA katika kuboresha miundombinu ya elimu Wilayani humo, Shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa karibu na serikali na jamii katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kwa kujenga na kukarabati madarasa, pamoja na kuweka vifaa vya kisasa katika shule za msingi na sekondari pamoja na miundombinu ya maji.
Akizungumza Oktoba 18, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, vyoo na kisima cha maji katika shule ya Msingi Makuture, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuf Makunja ameeleza kuwa juhudi hizi zinalenga kuongeza kiwango cha elimu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea.
"Mchango wa Shirika la SAWA unasaidia sana kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi katika upatikanaji wa elimu bora." amesema Mhe. Makunja.
Aidha, amebainisha kuwa shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na ukosefu wa maji safi hivyo kusababisha wanafunzi kutumia muda mwingi kutafuta maji kuliko masomo, pia amesema uhaba wa madarasa ulipelekea shule hiyo kuwa na vipindi viwili vya masomo yaani wanasoma asubuhi wengine mchana.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la SAWA Bi. Hellen Nkalang'ango ameeleza kuwa lengo lao ni kusaidia jamii za kipato cha chini kupata fursa sawa katika elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu huku akisisitiza kuwa shirika hilo litaendelea kujitolea katika kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kwa upande wao Wananchi wa Kitongoji cha Makuture ambao wanafaidika na mradi wa Shirika la SAWA wameeleza kuwa, maboresho hayo yameleta mabadiliko makubwa katika mazingira ya shule na hamasa kwa wanafunzi kuzingatia masomo.
Pamoja na mradi huo Shirika la SAWA limekabidhi mradi wa kisima cha maji, madarasa mawili, ofisi moja na vyoo katika shule msingi shikizi ya Mtakuja.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.