Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro imeipongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA Wilayani Mvomero kwa jitihada zake za kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa Wananchi wa Kata ya Mangae.
Pongezi hizo zimetolewa Septemba 29, 2024 na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Ndugu Solomon Kasaba, wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Wilayani Mvomero.
Ndugu Kasaba amesema RUWASA imeleta suluhisho la kudumu kwa changamoto za maji zinazo wakabili wakazi wa Kata ya Mangae kwa muda mrefu. Amebainisha kuwa juhudi hizo zina akisi dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na maeneo yao.
"...kwa uamuzi mliouchukua kabla ya mradi kukamilika kupunguza makali watu waanze kupata maji, tunawapongeza sana..." amesema Ndugu Kasaba.
Aidha, Katibu huyo wa CCM amewataka wananchi waendelee kuunga mkono juhudi za serikali na taasisi zake katika kutatua changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza wananchi kuutunza mradi huo ili udumu akibainisha kuwa CCM itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha mafanikio yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mvomero Mhandisi Mlenge amesema mradi huo umefikia asilimia 78 huku akisema kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 14. Aidha amesema mradi huo unagharimu kiasi cha milioni 643.
Nao wananchi wa Kata ya Mangae wameishukuru Serikali kwa mradi huo wa maji ambao utawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika maeneo mengine.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Morogoro inaendelea na ziara zake katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020.
MWISO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.