Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewapongeza walimu wa mkoa huo kwa kujitolea na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kitaifa zinazofanyika Mkoani humo.
Akizungumza Novemba 30, 2024 katika Bonanza la Mwalimu Day lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Morogoro
Dkt. Mussa ameelezea furaha yake kwa mchango mkubwa wa walimu katika mafanikio ya shughuli hizo.
"...ninawashukuru kwa sababu walimu ndani ya mkoa wa morogoro mmekuwa ni watu wa mbele katika kutekeleza mambo ya kitaifa..." amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Katibu Tawala huyo ameongeza kuwa walimu hao hushiriki shughuli hizo za kitaifa kwa ufanisi na hatimaye kuleta mafanikio.
Sambamba na hilo, Dkt. Mussa ameupongeza uongozi wa Chama cha Walimu Tanzania - CWT Mkoani Morogoro kwa kuandaa Bonanza hilo ambalo limewakutanisha walimu kutoka Halmashauri za Mkoa huo, huku akiwataka kuendeleza utaratibu huo wa mabonanza.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa pete, kuvuta kamba na riadha, hata hivyo bonanza lilihitimishwa kwa kutoa zawada kwa washindi mbalimbali waliopatikana kwenye mashindano ya bonanza hilo.
Halmashauri zilizoshiriki ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Ulanga, Kilosa, Gairo na Ifakara TC.
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imekuwa bingwa wa mashindano upande wa mpira wa miguu huku ikishika nafasi ya pili na ya tatu katika riadha.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.