Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi Mkoani humo Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa wito kwa waandikishaji wa wapiga kura wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanawahi kufika vituoni kwa wakati ili kuimarisha mchakato wa uandikishaji wa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakao fanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Dkt. Mussa ametoa wito huo Oktoba 08, 2024 wakati wa Semina ya Waandikishaji wa Wapiga kura kutoka Tarafa za Mgeta na Mlali iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Mzumbe.
Katibu Tawala huyo amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kurahisisha zoezi zima la kuandikisha wapiga kura kwa ufanisi, kuhakikisha kuwa hakuna ucheleweshaji unaoweza kuathiri zoezi hilo muhimu kwa demokrasia.
"...neno langu la kwanza ninaloliona sisi tufike katika vituo mapema..." amesema Dkt. Mussa
Ameongeza kuwa kufika mapema kutasaidia kuepusha msongamano katika vituo na kuleta usawa kwa wapiga kura wote wanaotaka kujiandikisha na kupiga kura.
Pamoja na hayo Dkt. Mussa amewasisitiza waandikishaji hao kuhakikisha kuwa vifaa vinavyohitajika katika zoezi hilo la uandikishaji vinakuwepo katika vituo vyao kwa idadi inayohitajika, amewataka kuwa wasiri na kuzingatia taratibu ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linakamilika kwa mafanikio. Pia amewataka kuwa na lugha nzuri kwa wananchi watakaofika vituoni kujiandikisha.
Naye, Msimamizi msaidizi wa Uchaguzi Mkoa wa Morogoro Bw. Jacob Kayange amebainisha kuwa jukumu kubwa la waandikishaji hao ni kuandikisha wananchi wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akisema kuwa vituo vya uandikishaji na kupiga kura vitakuwepo katika kila kitongoji.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Mary Kayowa amemuahidi Katibu Tawala huyo kuwa Mvomero imejipanga kuhakikisha kuwa maelekezo, miongozo na taratibu inasimamiwa ipasavyo ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi. Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yalianza Oktoba 07 kwa washiriki kutoka Tarafa za Mvomero na Turiani huku akibainisha kuwa kwa Tarafa za Mgeta na Mlali zinajumla ya washiriki 371.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.