Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha dhamira thabiti ya kuboresha maisha ya wafugaji nchini kwa kutoa Shilingi Bilioni 216 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya mifugo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hadi mwaka 2029.
Hayo yamebainishwa Julai 10, 2025 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati akizungumza na wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo katika Mkoa wa Morogoro, iliyofanyika katika Kijiji cha Kambala Wilayani Mvomero.
Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi, amesema kuwa fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, ununuzi wa vishikwambi, pikipiki kwa ajili ya maafisa mifugo ambapo kwa mwaka huu jumla ya shilingi bilioni 69.2 zimetolewa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.
“...mama karidhia sasa tutekeleze mpango wa uboreshaji wa Sekta ya mifugo kwa miaka mitano mfululizo na tunaanza na mwaka huu 2025...2029 tutahitimisha mpango wa maboresho kimapinduzi sekta ya mifugo...” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, amebainisha kuwa kampeni hiyo ya chanjo Pamoja na utambuzi linafanyika nchi nzima ambapo jumla ya ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17 na kuku milioni 40 watatambuliwa na kuchanjwa huku akiwataka wafugaji kujitokeza kwa wingi ili mifugo yao iweze kupata chanjo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuwa Mkoa huo umepokea chanjo ya CBPP 707000 kwa ajili ya ng’ombe 815,051, chanjo ya PPR 847,500 kwa ajili ya mbuzi na kondoo 737,673 na chanjo ya kuku 999000 kwa ajili ya kuku 1,654,617. Ameongeza kuwa jumla ya heleni 188000 kwa ajili ya ng’ombe na heleni 177500 kwa ajili ya mbuzi na kondoo.
Kwa upande wake Chifu Kashu Moreto ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza suala la chanjo na utambuzi wa mifugo hukua akisema kwa wamelipokea kwa mikono miwili.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.