Uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya mkoani Morogoro umeendelea kuleta mabadiliko chanya, ikiwemo kupungua kwa vifo vya mama na mtoto.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali imejenga, kukarabati na kuboresha vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, ikiwemo hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati, jambo ambalo limeongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi hata wa maeneo ya vijijini.
Akizungumza Julai 29, 2025 kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka 5 katika Mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha Aprili - Juni 2025, Katibu Tawala Wilaya ya Mvomero Bw. Said Nguya amepongeza juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya.
Aidha, ameongeza kuwa uwekezaji huo umesaidia kupungua kwa vifo vinvyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka 5 katika Mkoa wa Morogoro kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Magoma amesema kuwa mikakati ya Mkoa huo ni kuendelea kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga kwa asilimia 50 huku akiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuajiri Madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi ili kufikia malengo hayo.
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Phillipina Phillipo amesema kuwa Halmashauri hiyo imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 8 hadi kifo kimoja kwa kipindi cha Aprili - Juni 2025 hali hiyo imechangiwa na uwepo wa miundombinu bora ya huduma za Afya Wilayani humo.
Kikao kazi hicho ambacho kinafanyika katika ukumbi wa Prof. Kuzilwa uliopo katika Kata ya Mzumbe kitaendelea hadi Julai 31, 2025.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.